Mkamu mwenyekiti wa klabu ya Young Africans Fredrick Mwakalebela amewaomba radhi viongozi wa Simba SC, kufuatia kauli yake aliyoitoa jana kwenye baadhi ya vyombo vya habari kwa kudai amefanya mazungumzo na kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama na kumuhakikishia amesaliwa na mkataba wa miezi sita.
Mwakalebela alijimwambafai katika vyombo hivyo vya habari ikiwa ni sehemu ya kutuma salamu kwa Simba SC ambayo inammiliki kiungo huyo, kwa kuamini watamsajili mwishoni mwa msimu huu, kwa lengo la kukiimarisha kikosi chao.
Kufuatia taarifa za sakata hilo kusambaa na kupewa nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii, huku viongozi wa Simba wakiahidi kuishtaki Young Africans TFF na FIFA kwa kosa la kuzungumza na mchezaji mwenye mkataba, kiongozi huyo amelazimika kuomba radhi na kusambaza sauti yake katika mitandao ya kijamii kwa kusema alikua akifanya utani.
“Ninaiomba radhi klabu ya Simba na wanachama wangu wa Young Africans kwa kusema nimeongea na kiungo wa Simba Clautos Chama kwa ajili ya kumsajili.”
“Ilikuwa ni utani tu, sikuongea na mchezaji huyo, ilikuwa ni kuwapa pressure Simba kama wao walivyofanya kwa Tshishimbi. Naahidi hili halitatokea tena” amesema Mwakalebela.
Hata hivyo tayari Chama ameshakanusha kufanya mazungumzo na viongozi wa Young Africans na kuwataka mashabiki wa Simba kuwa watulivu, kwani bado ni mchezaji wao halali na ataendelea kuwepo klabuni hapo kwa mujibu wa makataba wake.
Chama kwa sasa yupo nchini kwao Zambia akisubiri wito wa kurejea nchini kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya michezo iliyosalia ya ligi kuu ya soka Tanzania bara, ambayo imesimama kupisha janga la maambukizi ya virusi vya Corona.