Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vitaendelea kufungwa hadi Serikali itakapotoa tamko lingine.
Ameyasema hayo leo, Aprili 14, 2020 katika kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Uratibu wa Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Homa ya Mapafu unaosababishwa na virusi vipya vya corona (covid-19).
Aidha, kupitia taarifa ya kikao hicho iliyotolea na Ofisi ya Waziri Mkuu, kiongozi huyo pia amesema kuwa Sherehe za Maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zinazofanyika kila Aprili 26 na Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani inayofanyika kila Mei Mosi, zote zimeahirishwa ikiwa ni hatua ya kuepusha misongamano.
Amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameelekeza kiasi cha Shilingi Milioni 500 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kutumika kwenye sherehe za miaka 56 ya Muungano ziwekwe kwenye mfuko wa kupambana na maambukizi ya covid-19 wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa hadi leo, Aprili 14, 2020 kuna visa 53 nchini, ikiwa ni ongezeko la visa vinne ambavyo vyote vimeripotiwa jijini Dar es Salaam.
Ametoa wito kwa wananchi kujitahidi kuepuka maambukizi ya virusi vya corona ikiwa ni pamoja na kutulia majumbani kwao kama sio lazima kutoka.
Pia, ametaka wadau kuendelea kutoa michango yao kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya virusi vya corona nchini.
Waziri Mkuu ameagiza elimu zaidi ya kujikinga itolewe kwa wananchi hasa wa mkoa wa Dar es Salaam unaoongoza kwa visa vya corona na Zanzibar.