Mshambuliaji na nahodha wa zamani wa kikosi cha mabingwa wa Tanzania bara Wekundu Wa Msimbazi Simba, Musa Hassan ‘Mgosi’ amesema winga Luis Miquissone anaitendea haki jezi yake, anapokua kwenye majukumu ya kuhakikisha alama tatu zinapatikana uwanjani.
Mgosi ambaye alikuwa anavaa jezi namba 11 ambayo anaitumia mchezaji huyo raia wa Msumbiji amesema tangu atundike daruga mwaka 2016 hakuna mchezaji aliyeitumia vyema namba hiyo kama anavyofanya Luis. Tangu Mgosi aondoke jezi hiyo imewahi kuvaliwa na Laudit Mavugo, Marcel Kaheza na Wilker da Silva.
Amesema jambo hilo pekee limefanya ajione amerejea upya uwanjani kutokana na kiwango cha nyota ambaye amefunga magoli matatu hadi sasa tangu asajiliwe wakati wa dirisha dogo la usajili msimu huu.
Luis ameonekana kuwapa raha mashabiki wa timu hiyo, huku wakitarajia kuona makubwa zaidi kwake kama alivyoahidi bado hajafikia kiwango anachokitaka.
“Hakuna mchezaji duniani kote ambaye akistaafu atafurahia jezi yake ikivaliwa na mtu mwenye kiwango duni, wakati yeye alikuwa kwenye uwezo mkubwa.”
“Ndio maana nasema wachezaji wa zamani waulize watakwambia maana kuna wakati wachezaji wakicheza kiwango cha chini, wanatamani waingie wawaonyeshe ufundi ila nyakati zinakuwa zimewatupa mkono, akili zinataka miili haipo tayari,” anasema Mgosi ambaye kwa sasa ni kocha wa kikosi cha Simba Queens kinachoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake.
Alizitaja sifa za mchezaji huyo kwamba ndani yake ana uzalendo licha ya kuipa thamani kazi yake pia amekuwa akijitoa mpaka tone la mwisho timu ipate matokeo.
“Kikubwa ajiepushe na vitu vitakavyoweza kumuondoa kwenye mstari, asione anajua ama amefika anapaswa kuendelea kujifunza na kutaka kufika mbali.
“Tangu niivue jezi yangu, Luis anaitendea haki, kutokana na jinsi anavyojituma kuhakikisha timu inapata matokeo, kila ninapomuona napata faraja ya kipekee.”
“Ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni wanaoleta chachu kwenye soka la Tanzania anajua nini anakitaka soka, mpira ukiuheshimu utakuheshimu.”