Uongozi wa klabu ya Young Africans ukishirikiana na mdhamini wa timu hiyo, GSM, umezitaja timu za Afrika ambazo wataenda kufanya usajili wa wachezaji wa kimataifa ikiwa kama ahadi waliyoweka ya kukiboresha kikosi hicho kwa ajili ya kufanya vizuri msimu ujao.
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Mhandisi Hersi Said, hivi karibuni aliahidi kuwa wapo tayari kuifanya Young Africans kuwa tishio tena kwa kuhakikisha wanafanya usajili wa maana wa wachezaji wenye hadhi ya kuitumikia timu hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Young Africans, Afisa Muhamasishaji Antonio Nugaz, amesema katika mpango wa usajili wa wachezaji wa kimataifa kutoka Afrika, utafanyika katika timu kama Enyimba FC (Nigeria), UD Songo (Msumbiji), El Marreikh (Sudan), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Kaizer Chiefs (Afrika Kusini) na Etoile du Sahel (Tunisia).
“Tutafanya usajili wa wachezaji wa maana wa daraja B wa kimataifa kutoka katika timu kama Enyimba, UD Songo, El Marreikh, Mamelodi Sundowns na Kaizer Chiefs ambao tunaamini wataifanya Young Africans kuwa timu ya ushindani na inayocheza soka la kuvutia.
“Lakini pia tutahitaji kufanya usajili wa wachezaji wanaocheza ligi ya ndani ambao lazima wawe katika kiwango cha daraja A, hatutakuwa tayari kufanya usajili wa mchezaji wa ndani halafu akawe kwenye kiwango cha kawaida,” Alisema Antonio Nugaz.