China imeiomba Marekani kutimiza wajibu wake kwa shirika la afya ulimwenguni, WHO baada ya Rais Donald Trump kusimamisha ufadhili kwa shirika hilo akilituhumu kushindwa kulishughulikia ipasavyo janga la virusi vya corona.
Kwa mujibu wa DW Waziri wa mambo ya nje wa China Zhao Lijian amewaambia waandishi wa habari alipozungumzia hali ya virusi hivyo ambavyo vimewaambukiza takribani watu milioni 2 kote ulimwenguni kwamba uamuzi huo wa Marekani huenda ukaathiri mataifa yote ulimwenguni.
Naye Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas amezungumzia uamuzi huo wa Marekani akisema uimarishwaji wa shirika hilo ni moja ya uwekezaji muhimu.
Maas ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba lawama hazitasaidia kwa kuwa virusi hivyo havina mipaka.
Ikumbukwe kuwa WHO, ilitenga kiasi cha dola milioni 675 kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ambapo limeripotiwa kuwa litaongeza fedha hizo hadi karibu dola bilioni moja.