Mshambuliaji wa Namungo FC Reliants Lusajo ameweka pembeni taratibu za kusaini mkataba mpya ndani ya klabu hiyo inayoshiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa mara ya kwanza msimu huu.

Lusajo ambaye ameonyesha umahiri mkubwa na kuisaidia Namungo FC kushika nafasi ya nne hadi kipindi hiki ambacho ligi kuu imesimama kupisha mapambano dhidi ya virusi vya Corona, anapewa nafasi ya kuanza kufikiria suala la mkataba mpya itakapofika mwishoni mwa msimu huu.

Mwenyekiti wa Namungo FC, Hassan Zidadu ameeleza kuwa, wameanza mazungumzo na nyota wao watatu ambao wanawindwa na klabu za Simba, Young Africans na Azam FC, na wanamtumaini ya kufanikisha mpango wa kuwasainisha mikataba mipya.

Kiongozi huyo amesema wakati mazungumzo na Lucas Kikoti na Bigirimana Blaise yakienda vizuri, Lusajo yeye ametaka mchakato wa mkataba mpya uanze mwishoni mwa msimu huu.

Hata hivyo tayari mshambuliaji huyo ameshaanza kuhusishwa na tetesi za kuwa kwenye mchakato wa kusajiliwa na klabu ya Young Africans, ambayo imedhamiria kukiimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao.

Lusajo ambaye ameifungia Namungo FC mabao 11 msimu huu anatajwa kukaribia kutua Jangwani kwa mara ya pili, kwani aliwahi kupita mitaa hiyo mwaka 2013.

Lusajo amekuwa katika kiwango bora tangu alipojiunga na Namungo ambapo msimu uliopita alichangia kuipandisha timu hiyo daraja baada ya kuifungia mabao 15.

Ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa ligi daraja la kwanza msimu uliopita ambao ndio walipanda ligi kuu.

Deo Mutta awafunda wanayanga
Bongani Zungu alivyoshindwa kulipa fadhila