Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema ni marufuku kwa watoto kukusanyika katika madrasa na shule za jumapili kwa watoto maarufu kama Sunday School kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19 ambapo bado watoto wamekuwa wakienda makanisani na misikitini kwa ajili ya kujifunza.

Waziri amesema kuwa alipokutana na maaskofu na mashehe walikubaliana kusitisha huduma nyingine zote isipokuwa ibada tu hivyo amepiga marufuku hiyo na kusema kwamba makanisa na misikiti itumike kwa shughuli za ibada pekee za kuliombea taifa tena kwa muda mfupi na baada ya ibada waumini watawanyike mara moja.

“Ninazo taarifa kwamba wameanzisha mfumo wa kupeleka watoto kwenye madarasa ya dini maarufu kama Sunday Schools. Tumeruhusu ibada tu, na hizo ibada lazima ziangaliwe ziwe za muda mfupi kadri inavyowezekana. “

“Tumesisitiza kwenye makanisa au misikiti ambako ibada zinafanyika, waumini wakae kwa kuachiana nafasi,” alisema Majaliwa jana.

Ameongeza kwamba  changamoto inajitokeza kwenye makanisa makubwa ambayo yana waumini karibu 3,000 na kweli,  “Hayo sasa yatakuwa ni makongamano. Tunaaamini maaskofu na mufti wataliweka vizuri suala hili la sunday school na madrassa,” amesema.

Amesema serikali haitazuia biashara kwenye masoko, maduka au supermarkets isipokuwa amewataka wenye biashara hizo wahakikishe wanaweka ndoo za maji na sabuni ili wateja wanawe mikono kabla ya kuingia kupata huduma na wakati wanapotoka kupatiwa huduma hizo.

Kuhusu mikusanyiko mingine,  amesema watu wanapaswa wajizuie kwenda kuzagaa kwenye vituo vya mabasi na kama hawana shughuli za lazima za kufanya huko, basi wabakie majumbani kwao.

Azam FC: Mdogo mdogo tunakuja
Mwanza: Wafungwa wauawa wakitoroka gerezani