Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed ametangaza ongezeko la wagonjwa wengine 6 waliokutwa na maambukizi ya Virusi vya Corona na kufanya idadi ya wagonjwa kisiwani hapo kufikia 24.
Ambapo amesema wagonjwa wote ni raia wa Tanzania wakiwemo wanaume watano na mwanamke mmoja ambao hawana historia ya kusafiri nje ya nchi siku za hivi karibuni.
Idadi hiyo inafanya hadi sasa Tanzania kuwa na idadi ya visa 94 kufuatia tangazo lililotolewa saa 24 zilizopita baada ya kutangazwa ongezeko la wagonjwa 29 wapya nchini humo.
Waziri amesema tayari wagonjwa wote wamelazwa katika vituo maalum kwa lengo la kuendelea kupata matibabu
Serikali ya kisiwa hicho inaendelea kuwasisitizia wananchi kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo zinazotolewa mara kwa mara ikiwemo kunawa mikono.
Vilevile imewaomba wananchi wenye dalili za homa kali , kukohowa na kupiga chafya kujitokeaza katika vituo vya Afya kwa vipimo zaidi.