Kwa mara ya kwanza, Italia imezinduwa programu ya simu za mkononi inayoweza kufuatilia maambukizi ya kirusi cha corona, wakati ikijitayarisha kuondosha zuio la shughuli za kawaida za kimaisha mwezi ujao.
Umoja wa Ulaya ulipendekeza matumizi ya programu za simu za mikononi kama sehemu ya mpango wa kuzisaidia nchi kulegeza marufuku, ambazo zimeuporomosha uchumi kwenye Umoja huo.
Kamishna wa Kirusi cha Corona wa Italia, Domenico Arcuri, alisaini sheria maalum hapo jana, ambayo imetoa mkataba wa kuendesha programu hiyo kwa kampuni moja mjini Milan.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, programu hiyo haitaweka hadharani majina wala maeneo waliyo watu, lakini itaweza kufuatilia maambukizi popote yalipo.
Mataifa kama Israel na Korea Kusini yamekuwa yakitumia programu hizo ambazo zinawasaidia watu kujuwa ikiwa wamekaa karibu na mtu mwenye maambukizi ya kirusi cha corona.