Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda ametoa maagizo makubwa manne kwa wakazi wa Jiji la Dar es salaam juu ya kujikinga na ugonjwa wa corona ambao sasa umekuwa janga la dunia.
Makonda amesema kuanzia sasa ni lazima wakazi wa jiji lake wavae barakoa kila wanapokwenda ili kujikinga na ugonjwa huo.
Maagizo hayo ni;
”La kwanza Kuanzia jumatatu kila anayepanda daladala na anayekwenda kwenye eneo la manunuzi ni lazima awe umevaa barakoa, ununue, ukate leso, ukate khanga, utafute lababendi ni lazima uwe umevaa”
”La pili kuanzia jumatatu biashara zote zifanyike katika mfumo wa take away, ukienda sehemu kanunue ondoka”.
”La tatu lazima kuwe na hatua au mita mbili katika kila pahala unapokwenda kwenye msongamano wa watu”
”La nne wenye masoko wote tafuteni mfumo mbadala mzuri wa kusimamia masoko yenu, haiwezekani kuwe na uongozi wa masoko lakini mnasubiri mpaka mkuu wa mkoa atoe kauli”.
Hayo yamezungumzwa leo Aprili 18, 2020 na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari, hayo yote ni katika kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa corona kwani hadi kufikia jana wagonjwa wa Corona wafikia 147, huku kukiwa na vifo 5.