Klabu ya Young Africans imesaini mkataba wa miaka miwili (2) na kampuni ya GSM, mkataba unaoifanya GSM kuzalisha na kuuza bidhaa mbalimbali zenye nembo ya klabu hiyo.
Awali GSM ilisaini mkataba na Young Africans kwa ajili ya kuzalisha na kuuza jezi tu, mkataba ambao bado upo hadi sasa. Mkataba huu mpya utawafanya mashabiki na wanachama wa Yanga kupata bidhaa nyingine kama track suits, bukta/pensi, scarfs, t-shirts, vikombe, key holders na vingine vingi.
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa kampuni ya GSM Mhandisi Saidi Hersi, amesema wanafurahi kupata fursa ya kutengeneza bidhaa nyingine zaidi kwa ajili ya klabu ya Young Africans. Amesema kumekuwa na uhitaji mkubwa wa bidhaa nyingine tofautitofauti ukiachana na jezi.
“Tukiwa kama wadhamini tunapenda kuona Young Africans ikipata mapato zaidi kupitia nembo yao. Kwa muda mrefu sasa klabu imekuwa ikipoteza mapato ambayo yamekuwa yakiishia kwenye mikono ya watu wachache.”
“Kwanza fikiria ni jezi ngapi zimeuzwa bila klabu kufaidika na matumizi ya nembo yao? Kumbuka wakati huo klabu ilikuwa inapata wakati mgumu kupata fedha kutoka vyanzo tofauti ili kuendesha shughuli zake za kila siku.”
Ameongeza kuwa, GSM wanataka kuiona Young Africans ikiwa imara kiuchumi.
“Tunahitaji kunufaika pia na udhamini wetu. Unawezaje kuuza bidhaa za klabu wakati mashabiki na wanachama hawafurahishwi na matokeo? Kwa hiyo matokeo mazuri ya timu yataleta chachu kwenye mauzo ya bidhaa za klabu hivyo watafurahia uwekezaji wetu.”
Hata hivyo Hersi amesema mashabiki na wanachama wameanza kuwa na imani na timu yao na kuona sasa inaweza kupigania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara au Kombe la Azam Federation Cup (FA) kwa msimu huu.