Wakala wa mshambuliaji wa mabingwa wa soka Tanzania bara Wekundu Wa Msimbazi Simba Meddie Kagere, amesema ameiweka kapuni ofa ya  klabu ya Levante, na kuamua ataendelea na kubaki Msimbazi.

Wakala wa mshambuliaji huyo anaeongoza kwenye orodha ya kupachika mabao msimu huu wa 2019/20, Patrick Gakumba alithibitisha taarifa za mchezaji wake kuhitajika nchini Hispania kwenye klabu ya Levante mwishoni mwa juma lililopita alipozungumza na moja ya chombo cha habari hapa nchini.

Gakumba amesema klabu ya Levante ilimuona Kagere kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Sevilla uliounguruma jijini Dar es salaam mwaka jana (2019) na kumalizika kwa kushuhudia Simba wakifungwa mabao matano kwa manne.

Hata hivyo amesema mipango ya mchezaji wake kujiunga na klabu hiyo imeshindikana kutokana na masharti yaliyowekwa. Amesema Levante walihitaji Kagere acheze michezo ya majaribio, lakini ameona mshambuliaji huyo sio wakucheza michezo ya majaribio, na pia dau waliloliweka halina hadhi ya kumuondoka Tanzania na kwenda Hispania.

“Ni kweli klabu ya Levante ya Hispania (La Liga) imeonyesha nia ya kumuhitaji mteja wangu Meddie Kagere, ila dau wanalotaka kutoa ni sawa na dau ambalo Boss Mo Dewji ameahidi kumpa, kwa hiyo sioni haja ya Kagere kwenda Hispania”

“Kwa ubora wa Meddie Kagere naamini anaweza kucheza hata Barcelona ama Real Madrid kwa kuwa anajua kufunga, na kama unavyojua kuwa washambuliaji wamekuwa adimu sana”-Patrick Gakumba-Meneja wa Meddie Kagere

“Meddie Kagere walianza kumuita mzee miaka mitano iliyopita na kila wanapomwambia anafunga na mimi ninachoangalia ni magoli na siangalii umri”. Aliongeza wakala wa mchezaji huyo.

Muhimbili yasambaza mavazi ya kukinga Corona wauguzi
Korea Kusini yakanusha Kim Jong Un 'wa Kaskazini' kufanyiwa upasuaji