Serikali ya Korea Kusini imekanusha taarifa zilizoenea mapema leo kuwa kiongozi wa nchi jirani ya Korea Kaskazini, Kim Jong-un yuko mahututi baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Taarifa hizo zilizoenea kwa kasi zilieleza kuwa Kim Jong-un alikuwa amepatwa na ‘upoozo wa ubongo’ baada ya upasuaji huo wa moyo, lakini hakuna chanzo kilichokuwa na uthibitisho.
Taarifa kutoka katika Ofisi ya Rais ya Korea Kusini iliyoko jijini Seoul imeeleza kuwa hakuna dalili zozote zinazoonesha kuwa kiongozi wa nchi hiyo jirani mwenye umri wa miaka 36 ni mgonjwa.
Imeeleza kuwa hakuna dalili zozote za mabadiliko ya hatua mbalimbali ndani ya Korea Kaskazini, na kwamba majirani zao hao wanaonekana wako katika hali ya kawaida.
Tetesi za kuwa kiongozi huyo ni mgonjwa ziliibuka baada ya kutohudhuria sherehe za maadhimisho ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya babu yake zilizofanyika Aprili 15, 2020.
Kim Jong-un hajawahi kutohudhuria sherehe hizo.