Wakati Kenya ikiwa nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kutangaza maamuzi ya kumaliza msimu wa soka 2019/20 kwa kuwatangaza Gor Mahia FC kuwa mabingwa, nchi nyingine za ukanda huo bado zipo kimya.
Kenya kupitia shirikisho la soka FKF lilitangaza maamuzi hayo jana, na kusambazwa katika mitandao ya kijamii, jambo ambalo limemaliza sintofahamu iliyokua imechukua nafasi kwa wadau wa soka nchini humo kuhusu mustakabali wa ligi yao, ambayo ilisimamishwa mwezi Machi, kwa ajili ya kupisha vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Hapa Tanzania pamekua na mjadala wa kufutwa kwa msimu ama kutangazwa kwa anaeongoza msimamo wa ligi kuu Tanzania bara (Simba SC) kuwa bingwa msimu huu, japo mijadala hiyo sio rasmi.
Wengine wamekua wakishauri suala la SUBRA kwani wanaamini huenda janga la Corona likamalizika siku za karibuni na burudani ya soka kupitia ligi kuu ikarejea, hivyo wanataka kuona bingwa akipatana baada ya kucheza mchezo yote 38.
Mmoja wa wadau wa soka nchini ambao wametetea hoja ya SUBRA ni Mkuu Wa Idara Ya Habari Na Mawasilino Wa Ruvu Shooting Masau Bwire, ambapo amesema hakuna haraka kwa TFF kumtangaza bingwa mapema kama walivyofanya Kenya hapo jana.
Masau amesema Tanzania kupitia shirikisho lake la soka TFF, bado ina muda wa kusubiri na kuona ukomo wa janga la Corona kama litamalizwa hivi karibuni, ama kuendelea kushika hatamu.
Mdau huyo anaamini endapo ligi itaendelea huenda Simba SC wakapoteza baadhi ya michezo yao iliyosalia na bingwa akawa mwingine, tofauti na wengi wanavyoendelea kuwapa nafasi kwa kuamini wanapaswa kukabidhiwa taji lao kwa sasa.
“Ni mapema sana kuamua bingwa kwa kuwa bado michezo haijaisha na ukizangatia Simba SC wanaweza wakapoteza na wachini yao wakachukua Ubingwa pia, vipi kuhusu Azam FC na Young Africans wanaomfuata”
“Kwa bahati nzuri Azam FC na Young Africans bado hawajakutana katika mchezo wa mzunguuko wa pili, hivyo lolote linaweza kutokea kwenye mchezo huo, na michezo mingine, ninaomba tufanye subra, tusiharakishe kumtangaza bingwa.” Alisema Masau
Kwa upande wa timu zinazoshuka daraja, Masau pia ametetea kwa kusema nazo zinapaswa kupata haki ya kumaliza michezo yote, ili kujua hatma yao, na kama maamuzi ya kumaliza msimu yataamuliwa kwa sasa kuna baadhi ya timu zitashushwa kimakosa.
Amesema timu zinazoshika mkia kwenye msimamo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara nyingi zina nafasi ya kujikwamua kwenye janga la kushuka, kutokana na kukaribiana kwa alama.
“Utamshushaje mtu ligi wakati yeye alikuwa na imani kuwa angeweza kupambana na akabakia kwenye ligi? ” Alihoji Masau
“Hili ni lazima tulitazame kwa jicho kubwa zaidi na tuangalie wanaojua soka zaidi na tuangalie walichofanya wenzetu ili tusilete manunguniko kwa wengine”
Ligi Kuu imesimama huku Simba SC wakiwa wanaongoza kwa pointi zao 71, wakifuatiwa na Azam FC pointi 54 baada ya wote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.