Makamu wa rais, Samia Suluhu Hassan, leo Mei 2, 2020 ameongoza wananchi, wanafamilia na viongozi mbalimbali katika mazishi ya aliyekuwa waziri wa katiba na sheria, balozi Augustine Mahiga yaliyofanyika kijijini kwao Tosamaganga Iringa.
Akitoa salamu za pole, amesema Serikali imepata pigo kubwa kwa kuondokewa na waziri mwenye uzoefu wa muda mrefu katika serikali na jumuiya za kimataifa.
Amesema marehemu Mahiga aliwakilisha vyema nchi yetu kimataifa kutokana na umahili wake katika diplomasia na hivyo aliitangaza vizuri nchi yetu.
Aidha mama Samia amesema kama alivyotangulia kusema kwenye salamu zake rais John Magufuli, Marehemu Mahiga alikuwa mnyenyekevu licha ya kushika nyadhifa mbalimbali hapa nchini.
Miongoni mwa viongozi wengine waliohudhuria mazishi ya balozi huyo ambayo yamegharamiwa na serikali kama alivyoagiza rais, ni Naibu spika, Tulia Ackson, Mkurugenzi mkuu idara ya usalama wa taifa, Diwani Athumani, Mbunge wa Ismani, William Lukuvi na mkuu wa mkoa wa Iringa, Ally Happy.