Watu 55 wamefariki dunia na wengine 16 wamejeruhiwa kwa mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa zilizonyesha jana nchini Rwanda.
Wizara inayoshughulia masuala ya dharura imeyataja maeneo ya Nyabihu, Gakenke, Muhanga, Musanze, Ruhango, na Rubavu kuwa ndiyo maeneo ya wilaya zilizoathirika zaidi.
“Mvua hizo pia zimeharibu nyumba 91, madaraja matano na kusomba hekari kadhaa za mashamba yenye mazao,” imeeleza taarifa ya Wizara.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Serikali itazisaidia familia za waathirika.
“Familia ambazo zimewapoteza wapendwa wao kwa mafuriko haya zitasaidiwa kuandaa mazishi, wale ambao wamejeruhiwa watapelekwa hospitalini na wale ambao bado wako kwenye maeneo hatarishi tunawatengea maeneo mengine yaliyopangwa,” imesema Wizara ya Udhibiti wa Masuala ya Dharura.
Waliopoteza maisha watazikwa leo, Mei 8, 2020 kwenye maeneo yao yatakayochaguliwa na ndugu, kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Wizara.