Ripoti ya ofisi ya Umoja wa mataifa inayoshughulikia masuala ya kiutu OCHA, imesema watu takribani 481,000 wamepoteza makaazi tangu kuanza kwa msimu wa mvua Afrika Mashariki mwezi Machi.
Mvua hizo zimesababisha mafuriko makubwa, maporomoko ya ardhi na uharibifu wa miundombinu katika mataifa ya Burundi, Kenya, Ethiopia, Rwanda, Somalia na Tanzania.
Watu zaidi ya milioni 1.3 katika ukanda wa Afrika Mashariki wameathirika na mvua kubwa zilizosabaisha mafuriko.
Imeelezwa kuwa nchini Uganda maji katika ziwa Victoria yameongezeka katika kiwango cha juu kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1994.
Mvua hizo kubwa zimechangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa katika bahari ya Hindi ambayo pia yanahusishwa na janga la moto nchini Australia.