Nahodha wa Watford Troy Deeney amesema hatarudi mazoezini kwa sababu anahitaji kulinda afya ya familia yake wakati huu wa janga la virusi vya Corona.
Deeney anasema hataki kumweka mtoto wake, ambaye amekuwa na shida ya upumuaji katika “hatari zaidi” na ameongeza kuwa hofu ni kubwa kutokana na takwimu kuonyesha nchini England watu wenye asili ya Afrika na Asia wanakufa zaidi kutokana na Virusi vya Corona.
Deeney amesema: “Tunahitajika kurudi wiki hii, nimesema sitaenda.” Pia klabu yake ya Watford haitarijii kuanza mazoezi Jumanne hii na inaeleweka klabu haina shida yoyote na msimamo wa nahodha wake Deeney.
Akiongea na Eddie Hearn na Tony Bellew kwenye kipindi cha The Talk YouTube, Deeney aliongezea: “Inachukua mtu mmoja kuambukizwa (virusi) ndani ya kikundi na sitaki kukipeleka nyumbani.
“Mwanangu ana miezi mitano tu, alikuwa na shida ya kupumua, kwa hivyo sitaki kurudi nyumbani kumweka kwenye hatari zaidi.”
Ofisi ya Takwimu za Kitaifa inasema wanaume na wanawake weusi wana uwezekano wa kufa mara mbili zaidi kutokana na virusi vya Corona ukilinganisha na watu weupe huko England na Wales.
Jana Jumanne klabu za Ligi Kuu England zinaanza mazoezi ya vikundi vya wachezaji watano kwa watano.