Ofisa miradi kutoka Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo (IVD), Dk. Furaha Kyesi amesema huduma za chanjo nchini hazijasitishwa bado zinaendelea kutolewa kulingana na ratiba za watoto walizopangiwa na kulingana na umri wao hata hivyo jambo la msingi ni kila mmoja kuhakikisha anajikinga kila anapompeleka mtoto.
Amesisitiza kuwa wazazi na walezi wanatakiwa kuzingatia kuavaa barakoa kila wanapowapeleka watoto wao hospitalini, vituo vya afya na zahanati kupatiwa huduma mbalimbali za kiafya ikiwamo zile za chanjo.
“Ukiwa umevaa barakoa inasaidia kukukinga lakini pia unawakinga na wale wanaokuzunguka, vile vile mnapofika kituoni zingatieni kunawa mikono na kukaa umbali wa mita moja, hakikisha unapokaa mkono wako ukiunyoosha hauwezi kugusa bega la mwenzako aliye pembeni yako,” amesisitiza Dk. Kyesi.
Hayo yamejiri wakati maofisa wa mpango huo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa mkoa wa Morogoro na wa Manispaa wako katika ziara ya kukagua utoaji huduma za chanjo katika Mkoa huo kwa kushirikiana na Shirika la Engender Health kupitia Merck Sharp & Dohme B.V (MSD).