Mshambuliaji wa FC Lupopo ya DR Congo Mpiana Monzizi amefichua kuwa anasubiri kumalizika changamoto ya Corona ili aweze kuja nchini kujiunga na mabingwa wa kihistoria, Young Africans.

Monzizi aliibuka mfungaji bora wa ligi kuu ya DR Congo akifungana na Jackson Muleka na Fiston Mayeke wa AS Vita wote wakifunga mabao 12.

Hivi karibuni nahodha wa Young Africans Papy Tshishimbi alifichua uwezekano wa klabu hiyo kumsajili mshambuliaji huyo ambaye pia ni raia wa DR Congo.

Monzinzi amenukuliwa na gazeti Mwanaspoti akithibitisha kufanya mazungumzo na Young Africans huku akibainisha kuwa kilichobaki ni kwake kusaini mkataba: “Tulishazungumza kila kitu na kufikia makubaliano, Kilichobaki ni kumalizana ili tujue msimu ujao tunauanzaje,”

“Tunasubiri ndege zianze kutembea pengine baada ya hii Corona naweza kuja Tanzania kusaini mkataba. Nimekuwa nikizungumza mara kwa mara na Tshishimbi akiniambia mambo mengi kuhusu ligi ya Tanzania. Sioni kama nitashindwa kufanya vizuri.”

Monzizi ni miongoni mwa washambuliaji wa DR Congo ambao wanatajwa kuwaniwa na Young Africans, wengine ni Heritier Makambo na winga Tusila Kisinda ambaye naye inaelezwa dili lake limefika pazuri.

DR Congo imemaliza msimu kwa kuwapa ubingwa TP Mazembe ambao walikuwa wakiongoza ligi kwa tofauti ya alama 12 ligi iliposimama miezi miwili iliyopita.

Dilunga kubaki Simba SC kwa miaka miwili
Troy Deeney: Sitarudi kwenye mazoezi!!