Kocha wa mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC, Sven Vandenbroeck amepanga kukiwezesha kikosi chake kushinda michezo yote iliyosalia, na kutetea ubingwa kwa heshima.
Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 13 kufuatia Serikali kuruhusu masuala ya michezo kuanza kuanzia leo, Juni Mosi, huku mabingwa hao wakisaliwa na michezo dhidi ya Ruvu Shooting, Mwadui FC, Mbeya City Na Tanzania Prisons.
Michezo mingine ni dhidi ya Ndanda FC, Namungo FC, Mbao FC, Alliance FC, Coastal Union na Polisi Tanzania.
Kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji amesema, mipango aliojiwekea ni kuhakikisha kikosi chake kinapata alama 15 katika michezo mitano ya mwanzo, ili kufikia lengo la kutetea ubingwa.
Amesema mbali na alama 15, pia amedhamiria heshima ya kuendeleza ushindi kikosini kwake, ili kujiongezea alama zitakazo dhihirisha ubora wa kikosi chake msimu huu wa 2019/20.
“Mipango ya timu ni kuhakikisha tunapata alama 15 katika michezo yetu mitano ya mwanzo ili kutwaa ubingwa wa Ligi mapema, pia tutafanikisha harakati za kushinda michezo mingine ili kujiwekea heshima ya kupata alama nyingine zitakazoweka historia ndani ya kikosi chetu.”
Ikiwa Simba SC watafanikiwa kupata alama 15 za michezo mitano ya awali watafikisha alama 86 ambazo haziwezi kufikia na timu yoyote ndani ya Ligi. Kwa sasa wababe hao wa Msimbazi wana alama 71.