Siku kadhaa zikisalia kabla ya kuendelea kwa mshike mshike wa Ligi Kuu ya England (EPL), masharti mapya yamewekwa ikiwa ni miongoni mwa hatua za kupunguza uwezekano wa kuibuka na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Corona.
Miongoni mwa masharti hayo ni uwepo wa watu wasiozidi 300 viwanjani ambao ni wachezaji, makocha, maofisa wa timu na wale wa chama cha soka, waamuzi, waokota mipira na wafanyakazi wa viwanja.
Kati ya watu hao 300 ni watu 105 tu ambao wataruhusiwa kuwepo katika eneo la kuchezea na pia kwenye eneo la wachezaji kuingilia uwanjani.
Sharti jingine ni makocha wa timu kutakiwa kufanya mikutano ya waandishi wa habari kabla au baada ya mechi kwa njia ya video badala ya utaratibu wa kawaida wa kuzungumza nao moja kwa moja.
La tatu ni waamuzi waliopo katika teknolojia ya usaidizi wa video (VAR) kila mmoja kukaa katika chumba chake tofauti na mwanzo ambapo walikuwa wanakaa chumba kimoja.
Ukiondoa hayo, pia kila timu itaruhusiwa kuwa na wachezaji 20 uwanjani badala ya 18 kama ilivyokuwa hapo awali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyofichuliwa na mtandao wa Daily Mail, waandishi wa habari wanaoruhusiwa kwa mchezo mmoja hawatakiwi kuzidi 40. Ligi Kuu ya England inatarajiwa kurejea Juni 17 ambapo kutakuwa na mechi mbili.
Mechi moja itakuwa ni baina ya Arsenal na Manchester City na nyingine itakuwa baina ya Aston Villa na Sheffield United.
Liverpool inaongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 82 na inahitaji ushindi wa mechi tatu tu kati ya tisa ilizobakiza ili iweze kutwaa ubingwa wa msimu huu.