Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli amewataka TANROAD mkoani Mbeya kuwalipa wananchi milioni 20 kwaajili ya kuendeleza ujenzi wa Shule katika eneo la Kata ya Isongole, Kijiji cha Isyonje ambapo eneo hilo lilikuwa limependekezwa kujengwa mradi wa mzani wa kupima uzito wa magari.
Amesema hayo kwa njia ya simu wakati akiongea na wananchi wa Isyonje ambapo alimtuma mkuu wa mkoa huo Albert Chalamila kufuatili mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka minne kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka 2020, kati ya wananchi na TANROAD.
”Nimeona wananchi walikuwa wana lalamikia Tanroad kupitia wizara ya ujenzi wamechukua eneo lao kwaajili ya kujenga mzani, mpaka leo hawajawalipa fidia nikaona huo ni upumbavu waambie wananchi waendelee na shughuli zao, hakuna mtu yeyote atakaye wasumbua” amesema Rais Magufuli
Ameongeza kuwa ”Hao Tanroad wawaache wananchi waendelee kufanya kazi zao na kujenga nyumba zao na kama ni mzani utajengwa mahali kwingine wasiwe wanawasumbua watu, kwa mujibu wa sheria ya ardhi kifungu namba 4 na namba 5 kinasisitiza kulipa fidia kabla hujachukua ardhi”
Aidha amewaomba radhi wananchi wa eneo hilo kwa kwa niaba ya watendaji wake kwa kuwacheleweshea maendeleo na kuwataka waendelee kufanya shughuli zao za kukuza uchumi wa Mkoa wa Mbeya.
Naye Mkuu wa mkoa wa Mbeya amesema “TANROAD kama mnataka kuchukua eneo la wananchi mjiandae mkiwa na hela ili wananchi wasisumbuke sasa kwakuwa mmejichelewesha, Rais wa nchi amesema wananchi wa eneo hili endeleni kujenga kulima na kufanya chochote”.