Mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, wametinga hatua ya fainali ya Kombe la Ujerumani (DFB-Pokal) kwa kuichakaza Eintracht Frankfurt mabao mawili kwa moja.

Mchezo huo wa nusu fainali ulikuwa na ushindani kwa timu zote huku kukiwa na piga nikupige tofauti na michezo ya ligi ambayo FC Bayern Munich wamekuwa wakishinda kiurahisi, tena kwa mabao mengi.

Kwa mantiki hiyo FC Bayern Munich watacheza dhidi ya Bayer 04 Leverkusen ambao nao walishinda mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Saarbrucken siku ya Jumanne.

Mpambano wa fainali umepangwa kupigwa Julai 04 kwenye dimba la Berlin Olympic.

Mshambuliaji wa Croatia Ivan Perisic alikuwa wa kwanza kufunga goli la kwanza kwa upande wa Munich lakini Eintracht Frankfurt mabingwa wa taji hilo mwaka 2018 waliimarika kipindi cha pili na kusawazisha kupitia kwa Danny da Costa.

Mshambuliaji kutoka nchini Poland Robert Lewandowski, aliipatia ushindi FC Bayern Munich kwa kumalizia pasi ya Mjerumani Joshua Kimmich, bao ambalo lilitakataliwa kwa minajali ulikuwa mchezo wa kuotea lakini video saidizi ya refarii ikaruhusu kuwa goli halali.

Lewandowski anafikisha mabao 45 katika michezo 39 ambazo amecheza katika michuano yote msimu huu wa 2019/20.

FC Bayern Munich, ambao wamebakiza ushindi wa michezo miwili ili kutawazwa mabingwa wa Bundesliga na kuwa taji la nane mfululizo, wameshinda michezo 20 kati ya 21 ambayo wamecheza kwenye michuano yote msimu huu.

JPM 'awajibu' wanaopanga kumuongezea muhula wa tatu madarakani
Vingozi wa vijiji matatani baada ya polisi kukamata hekari 100 za bangi