Polisi nchini Lesotho wamesema kuwa wana ushaidi kwamba aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Thomas Thabane na mke wake wa sasa Maesaiah walilipa majambazi kumuua mke wazamani wa Thabane mwaka 2017.
Polisi pia wanasema waziri mkuu huyo wa zamani na mke wake walidaiwa kuwalipa majambazi kima cha dola elfu 180 sawa na (£142,000) ambayo ilikuwa ilipwe kwa awamu.
Dola elfu 24 tayari zilikuwa zimelipwa, kwa mujibu wa stakabadhi hizo zilizo wasilishwa mahakamani chini ya kiapo huku Mmoja wa majambazi hao anatarajiwa kutoa ushahidi kwa niaba ya taifa.
Thabane ambaye amekana kuhusika na mauaji hayo alilazimika kujiuzulu mwezi uliopita kutokana na madai ya sakata hilo la mauaji. Bado hajafunguliwa mashitaka, lakini stakabadhi za polisi zinadai kuwa aliwaonesha majambazi nyumbani kwa mke wake wa zamani.
Mke wa sasa wa Thabane, ambaye anakabiliwa na mashitaka ya mauaji, amekuwa akizuiliwa tangu wiki iliyopita. Mawakili wake wanataka aachiliwe kwa dhamana ili akamhudumie mumewe mgonjwa jambo lililopingwa na maofisa wa pilisi.
Lipolelo Thabane alipigwa risasi akiwa kando ya barabara alipokuwa akirudi nyumbani katika kijiji kidogo kandokando ya mji mkuu wa Maseru na kuuawa, usiku wa kuamkia siku ya kuapishwa Thabane kuwa waziri mkuu.
A wali, alikabiliwa na talaka kutoka kwa Thabane wakati alipouawa. Wakati huo, waziri mkuu alikuwa akiishi na Maesaiah, mwenye umri wa miaka 42.
Kwa mujibu wa polisi, Bw. na Bi. Thabane walitaka kumuua, Lipolelo, ili mke wake wa sasa apate nafasi ya kuwa mama taifa.
Miezi miwili baadaye yeye na bwana Thabane walioana katika sherehe ya kikatoliki iliofanyika katika uwanja wa Maseru uliojaa.
Lakini muda mfupi kabla ya kifo chake, Lipolelo Thabane alishinda kesi mahakamani ya kuthibitisha kuwa yeye ndiye mama taifa halisi wa Lesotho na kwamba licha ya kuwa katika ya mgogoro wa kesi ya talaka bado alistahili kulipwa mafao yanayotokana na wadhifa huo.
Imeandikwa kwa hisani ya BBC swahili