Nahodha na Mshambuliaji wa Mabingwa wa Hispania FC Barcelona Lionel Messi, mwishoni mwa juma lililopita aliingia kwenye ramani nyingine ya soka duniani, baada ya kuifungia timu yake moja ya mabao manne dhidi ya Real Mallorca.

Messi alifunga bao la mwisho kabisa katika mchezo huo na kumfanya awe amefikisha mabao 20 kwenye La Liga msimu huu, akiongoza kwenye mbio za kusaka tuzo ya Mfungaji Bora nchini Hispania (Pichichi).

Lakini, bao hilo limelifanya jina lake kukaa kwenye chati za juu kabisa, akiwa mchezaji pekee kuwahi kutokea kwenye dunia ya mchezo wa soka kufikisha mabao 20 kwa misimu 12 mfululizo.

Messi anashikilia pia rekodi ya mabao kwenye La Liga na bado anaongeza nyingine kumfanya kuwa, mchezaji wa kupekee katika kuwahi kutoka kwenye ligi ya Hispania. Anatesa pia kwenye chati za kuasisti.

Alihusika kwenye kuwapikia wenzake katika mchezo huo wa Jumamosi na hivyo kumfanya awe amefikisha asisti 14 kwenye La Liga msimu huu.

Wafungaji wengine wa mabao ya Barcelona ni Arturo Vidal, Martin Braithwaite na Jordi Alba.

Ushindi huo uliifanya Barcelona kuweka pengo la pointi tano kileleni dhidi ya Real Madrid, ambao walikuwa na mechi jana Jumapili usiku kwa kumenyana na Eibar uwanjani Bernabeu.

Kocha wa Barcelona, Quique Setien alifurahia ushindi huo akisema kimekuwa kitu kizuri kuanza vizuri, baada ya ligi hiyo kusimama kwa miezi kadhaa kutokana na janga la Corona.

Ummy akemea matumizi mabaya ya simu kwa watoto "huchochea ngono"
Azam FC wamtema Donald Ngoma