Hatua iliyobaki ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya (UEFA Champions League) sasa itapigwa kwenye mji mmoja wa Lisbon nchini Ureno kwa muda wa siku 12 pekee, kuanzia Agosti 12 hadi Agosti 23 mwaka huu.
Kwa mujibu wa mapendekezo yaliyotolewa leo, hatua hiyo ya mtoano itapigwa katika viwanja viwili pekee kwa mechi mojamoja kuchezwa badala ya ule utaratibu wa mechi mbili yaani nyumbani na ugenini.
Kwa mujibu wa ratiba inayopendekezwa, mechi za robo fainali zitachezwa kati ya Agosti 12 hadi 15, nusu fainali zitakuwa Agosti 18 na 19 na fainali itachezwa Agosti 23. Viwanja vitakavyotumika ni Estadio da Luz na Estadio Jose Alvalade.
Timu zilizofuzu robo fainali hadi sasa ni Paris Saint-Germain, Atalanta, Atletico Madrid, RB Leipzig lakini bado kulikuwa na mechi nne ya marudiano zilikuwa hazijachezwa katika hatua ya 16 bora.
Mechi hizo ni (kwenye mabano ni matokeo ya mechi za mkondo wa kwanza)
Manchester City vs Real Madrid (2-1).
Bayern Munich vs Chelsea (3-0).
Juventus vs Lyon (0-1).
Barcelona vs Napoli (1-1).
Kamati ya Utendaji ya UEFA inatarajiwa kupitisha mapendekezo haya kesho Jumatano, Juni 17, 2020.