Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ameeleza sababu za kuwaondoa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqaro na aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dkt. Maulid Madeni.
Akizungumza leo, Juni 22, 2020 Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kuwaapisha viongozi wapya aliowateua kushika nafasi hizo, Rais Magufuli amesema kuwa alifanya uamuzi huo kwakuwa hakukuwa na maelewano baina yao.
“Mimi huwa nasikitika sana unapowaona watu uliowaapisha na kuwaamini kwa niaba ya Watanzania, wanapoenda kule hawafanyi kadiri ya viapo vyao. Arusha ilibidi nitengue uteuzi wa wote niliokuwa nimewateua, kuanzia RC, Mkurugenzi wa Jiji pamoja na DC,” amesema Rais Magufuli.
“Ni kwa sababu katika kipindi chote karibu miaka miwili walikuwa wanagombana tu, kila mmoja ni Boss, kila mmoja anatengeneza mizengwe ya wenzake, sikufurahishwa… walifanya kazi zao lakini waliniudhi wao kutoshirikiana na kutofanya yale niliyowaagiza,” aliongeza.
Rais Magufuli amewaeleza viongozi aliowaapisha kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano na kwa kuzingatia viapo vyao.
Walioapishwa leo ni Idd Kimanta ambaye amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenan Kihongosi anayekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha na Dkt. John Pima ambaye amekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha.