Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kutoa vibali vya kushiriki uchaguzi mkuu mwezi octoba mwaka huu kwa Asasi za kiraia 272 ambazo ziliomba kutoa elimu ya mpiga kura na zilizoomba kuwa watazamaji.
Mkurugenzi wa NEC, Wilison Mahera katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amesema kuwa tokea walipotangaza nafasi hizo 2019 hadi januari mwaka huu, mwitikio ulikuwa mkubwa japo kuna ambazo hazijakidhi sifa za kupata nafasi.
“Tume imepitia kwa kina na kufanya uchambuzi na kubaini kwamba asasi 245 zinazo sifa za kutoa elimu ya mpigakura, asasi nyingine 97 zimepata kibali cha kuwa watazamaji katika uchaguzi wa mwaka 2020” Amesema Mahera.
Kwaupande wa asasi ambazo hazijakidhi vigezo amesema zipo ambazo ziliomba nafasi lakini zimesajiliwa na msajili tofauti, zipo ambazo hazijafanikiwa kuonesha matumizi ya fedha na nyingine hazina ofisi.
Aidha amesema baada ya asasi zilizokubaliwa kupata barua zao, NEC itafanya kazi pamoja nao kama sheria inavyoelekeza na watawapa muongozo wa jinsi ya kufanya kazi ikiwepo kuwataka waoneshe vyanzo vya fedha watakavyozipata na watakavyotimia.