Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC Thabit Zakaria (Zaka Zakazi), ameungana na wadau wa soka Tanzania wanaoendelea kulaani rafu aliyofanyiwa beki wa pembeni wa Mabingwa wa Tanzania Bara Shomari Kapombe kwenye mchezo wa Robo Fainali Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC) uliochezwa jana usiku Uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Nahodha na kiungo wa Azam FC Frank Domayo alimchezea rafu mbaya beki huyo na kuzua taharuki kwa mashabiki waliokua wanafatilia mpambano huo uliomalizika kwa Simba SC kuibuka na ushindi wa maboa mawili kwa sifuri na kutinga hatua ya Nusu Fainali.
Zaka amekiri kitendo alichokifanya Domayo sio cha kiungwana, lakini amesisitiza mambo hayo hutokea katika soka, na ndio maana kiungo huyo amekua mwepesi kuomba radhi.
Hata hivyo Zaka amesema haoni sababu ya wadau wa soka nchini kuendelea kulikuza jambo hilo, kutokana na muhusika kuomba radhi hadharani, lakini anaamini kinachoendelea ni ushabiki ambao siku zote haujengi, zaidi ya kuongeza chuki.
Anaamini kosa hilo limeonekana kubwa sana kwa sababu limefanywa dhidi ya mchezaji wa Simba, lakini kosa kama hilo liliwahi kufanywa na Mohamed Ibrahim wa Simba dhidi ya Kapombe akiwa Azam FC, lakini mashabiki hawakusema lolote, zaidi ya kukaa kimya.
“Faulo ile ilikuwa mbaya Azam Kama Klabu hatujafurahishwa na faulo hiyo ni aina ya makosa yanayotokea katika mpira isikuzwe sana kwa sasa inakuzwa mno kwa kuwa ametendewa mchezaji wa Simba na wanaopiga kelele ni wengi”
“Mwaka 2017 Shomary Kapombe huyu huyu alikanyagwa tumboni kwa makusudi na Mohamed Ibrahim wa Simba watu walikuwa kimya kabisa kama hakikufanyika kitu tuache hizi double standard.
Leo Alhamis Kapombe anatarajiwa kufanyiwa vipimo ili kujua ukubwa wa tatizo lake kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandnbroeck.