Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC, Senzo Mazingiza Mbatha, amesema mchezo wa Nusu Fainali Kombe La Shirikisho (ASFC) dhidi ya Young Africans utakuwa ngumu na wamejiandaa kukabiliana na ushindani kutoka kwa watani zao.
Mbatha amesema wanajua Young Africans wataingia na presha ya kutaka ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao kupitia michuano ya ASFC.
Amesema kikosi chao hakitotaka kupoteza tena dhidi ya Young Africans, na kitaingia uwanjani kwa lengo la kulipa kisasi na kuhitaji heshima ya Ufalme wa soka la Tanzania, baada ya kutwaa taji la Ligi Kuu kwa mara ya tatu mfululizo.
“Itakuwa na ushindani kutoka pande zote mbili, kila timu itaingia kuhakikisha malengo yake yanafanikiwa, kwetu tumejipanga kuhakikisha haturudii makosa, kupoteza tena mchezo wa ‘dabi’ haiwezekani, tunahitaji kufanya nguvu ya ziada kama mabingwa,” amesema Mazingiza
Ameongeza anafurahi kuona msimu wake wa kwanza wameshinda taji la Ligi Kuu Tanzania Bara na anatarajia kukamilisha furaha ndani ya klabu hiyo kwa kulipa kisasi cha kuifunga Young Africans na kuiondoa kwenye kampeni ya kuwania kombe hilo la tatu msimu huu.
Kwa upande wa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo, Haji Sunday Manara, ameendelea kutamba kiosi chao kimeshachukua makombe matatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, sasa yamebaki saba katika mkakati wao wa kushinda mara 10 mfululizo.
Manara amewataka watani zao Young Africans pamoja na timu nyingine wasiweze mawazo ya kushinda taji hilo mpaka kuanzia mwaka 2027 ambapo wao wanaweza kuliachia.
Mbali na mchezo huo, Nusu Fainali nyingine ya ASFC itakuwa kati ya Namungo FC dhidi ya timu ya Daraja la kwanza, Sahare All Stars ya jijini, Tanga itakayochezwa kesho Jumamosi.