Makamu wa Rais, Samia Suluhu, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio za CRDB Marathon zitakazofanyika Agosti 16, mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa lengo la kukusanya fedha za kugharamia watoto wenye kuhitaji upasuaji wa moyo hapa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela aliwataja viongozi wengine watakaoshiriki mbio hizo ni pamoja na Rais mstaafu Jakaya Kikwete pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harisson Mwakyembe.
“Kauli mbiu yetu katika mbio hizi za hisani ni *Kasi Isambazayo Tabasamu*, ikihamasisha watu wengi zaidi kujitokeza kushiriki kuleta tumaini la maisha na kusambaza tabasamu kwa watoto wenye magonjwa ya moyo,” alisema Nsekela.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Profesa Mohamed Janabi, aliishukuru CRDB kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia jitihada za utoaji huduma za upasuaji moyo kwa watoto na kueleza asilimia moja ya watoto milioni mbili wanazaliwa na magonjwa ya moyo hapa.