Bingwa wa ulimwengu wa mbio za mita 1,500 mwaka wa 2017 Mkenya Elijah Manangoi, amefungiwa kushiriki michuano ya riadha dunaini baada ya kukataa kufanyiwa vipimo.
Kitengo cha Uadilifu katika mchezo wa Riadha duniani (AIU), kimetoa taarifa kuwa Manangoi alikataa kufanyiwa vipimo, baada ya kushukiwa huenda akawa anatumia dawa za kuongeza nguvu mwilini.
Manangoi mwenye umri wa miaka 27, alipokea medali yake ya fedha katika mashindano ya dunia Beijing 2015 kabla ya kushinda medali ya dhahabu jijini London miaka miwili baadae. Alijiondoa katika mashindano ya dunia mjini Doha mwaka wa 2019 siku chache kabla ya kuanza.
“Kile ninachosema ni kuwa kila kipimo nilichokosa kufanyiwa kilitokea mwaka wa 2019, kesi zangu hazihusiani na dawa zilizopigwa marufuku na kila mara nimeshiriki mashindanoni kama mwanariadha safi.
Mwaka jana ulikuwa mgumu sana katika taaluma yangu wakati niliathirika kupitia majeruhi ambayo yaliharibu kila kitu ndani na nje ya uwanja.
“Kwa sasa natayarisha jibu la kuwapa AIU kwahiyo sitaongea zaidi ya hayo.” Amesema Manangoi
Chini ya kanuni hizo, wanariadha lazima wawafahamishe maafisa kuhusu mahali walipo kwa siku 90, kabla ili kufanyiwa vipimo vya nje ya mashindano. Wanachukuliwa kuwa wamefanya kosa kama watashindwa kufanyiwa vipimo mara tatu.