Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Maka Mwalwisi, amewapongeza vijana wake kwa kazi kubwa walioifanya kwenye mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya mabingwa watetezi Simba SC.
Mchezo huo uliunguruma Jumapili Septemba 06, Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kushuhudia Ihefu FC wakiambulia kichapo cha mabao mawili kwa moja.
Mwalwisi amesema wachezaji wake walicheza vizuri, na wakati wote walifuata maelekezo aliowapa, lakini anaamini bahati ya ushindi haikua kwao siku hiyo.
Amesema kwa hakika wachezaji wake walicheza kwa kuwaheshimu sana Simba SC, na ndio maana mambo yaliwanyookea ndani ya dakika 90, lakini akasisitiza wazi kuwa endapo kikosi chake kisingetoa heshima hiyo huenda kingemaliza kwa kufungwa idadi kubwa ya mabao.
“Niliwaambia wachezaji wangu wacheze kwa kuwaheshimu Simba, lakini kwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza.”
“Kwa hilo tulifanikiwa na kuonyesha mchezo mzuri, hivyo kama tumeweza kuonyesha uwezo mkubwa kwa timu kama Simba, naamini mechi zijazo tutafanya vizuri zaidi,” amesema Mwalwisi.
Kwa sasa Ihefu FC wanaendelea na maandalizi ya mchezo wa mzunguuko wa pili Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya maafande wa Ruvu Shooting kutoka mkoani Pwani. Mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Sokione jijini Mbeya Septemba 13.