Mwendesha mashtaka mkuu wa Kenya, Noordin Haji, ameamuru kufanywa kwa uchunguzi wa dola milioni 71 zilizotengwa kwa ajili ya kukabiliana na janga la Corona ambazo zinadaiwa kutumika isivyo halali na Mamlaka ya Usambazaji wa Vifaa vya Tiba, KEMSA.
Wafanyakazi wa hospitali nchini humo wanaokabiliwa na hali ngumu katika utendaji kazi wao, wamefanya migomo wakipinga vitendo vya ufisadi katika mamlaka hiyo, ambayo hununua na kusambaza dawa na vifaa vya matibabu kwa ajili ya hospitali za umma nchini humo.
Wiki tatu zilizopita, Rais Uhuru Kenyatta aliitaka Tume ya Maadili na Vita Dhidi ya Ufisadi (EACC) ichunguze kandarasi zilizopewa watu mashuhuri, pamoja na wanasiasa, bila kuzingatia sheria za ununuzi wa umma.
Ripoti yake iliwasilishwa Ijumaa kwa mwendesha mashtaka, ambaye alihitimisha kuwa ulifanyika “ununuzi usiokuwa wa kawaida na malipo ya ulaghai” ya kiasi cha dola milioni 71.