Saa kadhaa zikiwa zimesalia kabla ya mtanange wa mzunguuko wanne wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba SC dhidi ya Gwambina FC, maneno ya tambo na tahadhari yameanza kusikika, huku kila upande ukiwa tayari kuzishambulia dakika 90.
Pambano hilo litachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam kesho Jumamosi, Septemba 26 saa moja usiku, huku Gwambina FC wakiwa na alama moja walioipata kwenye mchezo wa mzunguuko wa pili dhidi ya Kagera Sugar, wakipoteza dhidi ya Biashara United na Ruvu Shooting.
Simba SC ambao ni mabingwa watetezi wana alama saba zilizopatikana kwenye michezo mitatu, wakishinda dhidi ya Ihefu FC na Biashara Utd, huku wakilazimishwa sare ya bao moja kwa moja na Mtibwa Sugar.
Mkurugenzi wa ufundi wa Gwambina FC yenye maskani yake makuu wilayani Misungwi mkoani Mwanza, Mwinyi Zahera amesema mchezo dhidi Simba chochote kinaweza kikatokea kwani wapinzani wao ni timu kubwa nchini lakini kikosi chake kipo tayari kukabiliana nao kesho Jumamosi, Septemba 26.
Zahera amesema pamoja na ubora wa kikosi cha Simba SC kilichosheheni wachezaji wenye viwango vikubwa nchini, kamwe hawezi kutishika na ukubwa huo.
“Mimi nimeshacheza na Sadio Mane, Mohamed Salah lakini sikuwaogopa vipi nije kuwaogopa kina Kagere na Chama ingawa ni wachezaji wazuri, nawaheshimu lakini siwezi kuwaogopa.”
“Chama siwezi kumuogopa, ni mchezaji mkubwa na mzuri lakini hapana hatuwezi kumuogopa, tukisema kumuogopa hapo tunaenda mbali sana”
“Simba SC wanaweza kumuanzisha Kagere au hata wakamchukue Ronaldo kule Italia sisi hatutawaogopa, wana kikosi kizuri sana lakini kuwaogopa hiyo ni hatua kubwa. Nimewaona wachezaji wakubwa kuliko wao” Amesema Zahera.
Aidha, Kocha huyo amesema ili waone ukubwa wa Simba SC basi wawafunge zaidi ya mabao manane kwani hata FC Barcelona waliwahi kufungwa idadi hiyo ya mabao dhidi ya FC Buyern Munich ya Ujerumani katika nusu fainali ya Ligi ya mabingwa Barani Ulaya.
Itakumbukwa kuwa Mwinyi Zahera amewahi kuwa kocha mkuu wa Young Africans msimu wa 2018-19 kabla ya kutimuliwa mwishoni mwa mwaka jana kutokana na kuwa na matokeo mabaya yaliyomuandama.