Rais wa Marekani Donald Trump amemteua rasmi Jaji Amy Coney Barrett katika Mahakama Kuu kuziba pengo lililoachwa na jaji Ruth Bader Ginsburg aliyefariki dunia siku nane zilizopita akiwa na umri wa miaka 87.
Trump alitarajiwa kwa kiasi kikubwa kumteua Barrett mwenye umri wa miaka 48 na ambaye pia alikuwa chaguo la Republican kutokana na misimamo yake ya nyuma kuhusu masuala ya utoaji mimba, haki za matumizi ya silaha na uhamiaji.
“Huu ni uteuzi wangu wa tatu katika Mahakama Kuu na ni wakati mzuri,” amesema Trump akiwa katika bustani za Ikulu ya White House baada ya maneno machache ya kumshukuru Ruth Bader Ginsburg kwa kazi kubwa aliyoifanya.
“Usiku wa leo, nina furaha kubwa kumteua mmoja wa wanasheria mahiri na wenye vipaji zaidi nchini katika Mahakama Kuu, ujasiri wake mkubwa, uzoefu wake mzuri na uaminifu wake unaoendana na Katiba utakuwa vizuri,” amesisitiza Trump akimwambia jaji aliyesimama kando yake.
Barrett, karani wa jaji wa zamani wa marehemu jaji Antoni Scalia amesema baada ya uteuzi huo kwamba anaipenda Marekani pamoja na katiba yake na kuongeza kuwa jaji anatakiwa kuitumia sheria kama ilivyoandikwa na kwamba majaji si watunga sera.
Kulingana na taratibu, wateule wa mahakama ya juu ni lazima waidhinishwe kwa wingi wa kura katika bunge la Seneti ambalo kwa hivi sasa linadhibitiwa na Republican.
Kiongozi wa walio wengi katika Seneti Mitch McConnell, amemmwagia sifa Barrett kama “mteule aliyekidhi vigezo”, kauli ambayo imedhihirisha wazi kwamba bunge hilo litapitisha chaguo la Trump.