Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa muda wa siku 5 kuanzia Oktoba mosi hadi 5 mwaka huu ili kuwawezesha wanafunzi waliomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) hivi karibuni kuingia katika mfumo wa kuomba mkopo kwa njia ya mtandao na kukamilisha maombi yao.
Katika taarifa yake aliyotoa kwa vyombo vya habari leo Septemba 30, Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru alisema uamuzi huo unatokana na maombi ya wanafunzi, wazazi na walezi ambao hawakuweza kuomba au kukamilisha maombi yao kutokana na sababu ya kujiunga na mafunzo hayo.
Kwa mujibu wa Badru alisema katika muda huo wa siku tano, mfumo pia utakuwa wazi ili kuwawezesha waombaji ambao maombi yao yana upungufu kurekebisha kwa kuweka nyaraka sahihi ili kuiwezesha HESLB kuendelea na hatua nyingine.
“Kwa wanaorekebisha taarifa, wanapaswa kuingia katika akaunti zao walizofungua kuombea mkopo na watapata ujumbe kuhusu maeneo ya kurekebisha. Tunawasihi watumie muda huu wa siku tano kurekebisha na kukamilisha maombi yao’’ alisema Badru.
Katika mwaka wa masomo 2020/2021, Serikali imetenga fedha shilingi Bilioni 464 zitakazowanufaisha jumla ya wanafunzi 145,000, kati yao, wanafunzi 54,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza na wengine 91,000 ni wanafunzi wanufaika wanaoendelea na masomo.