Mshambuliaji wa Vinara wa Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Azam FC Prince Dube ameshindwa kujiunga na timu ya Taifa Zimbabwe kutokana na majeraha ya nyama ya paja.
Dube ambaye ni Kinara wa mabao wa ligi kuu Tanzania Bara, aliumia kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar, Jumapili (Oktoba 04), ambapo alitakiwa kuripoti kwenye kambi ya timu yake ya taifa Jana Jumanne (oktoba 06). Zimbabwe inajiandaa kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi, Oktoba 11 utakaochezwa jijini Blantryre – Malawi.
Daktari wa Klabu ya Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, amesema hali Mshambuliaji huyo siyo mbaya na amepewa mapumziko wa juma moja moja kabla ya kuanza mazoezi mepesi kisha arudi katika hali yake ya zamani.
Dube ameshapachika wavuni mabao matano, hatua inayomfanya kuwa kinara kwenye orodha ya wafungaji bora Ligi Kuu 2020/21, ambayo bado inaendelea.
Wakati Dube akiongoza orodha ya upachikaji mabao Ligi Kuu, mshambuliaji wa Simba SC Meddie Kagere anamfuatia kwa kufikisha mabao manne.