Siku moja baada ya kusitishiwa mkataba wa kufanya kazi na klabu ya Ihefu FC inayoshiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara, kocha Maka Mwalwisi ameeleza kwa undani sababu zilizopelekea kikosi cha klabu hiyo kushindwa kufurukuta kwenye michezo kadhaa waliyocheza tangu kuanza kwa msimu huu 2020/21.
Kocha Mwalwisi ambaye alifaniksha Ihefu FC kucheza Ligi Kuu ikitokea Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2019/20, amesema imekua kama bahati mbaya kuondolewa kwenye nafasi yake, lakini alikua amejipanga kufanya makubwa akiwa na klabu hiyo ya mkoani Mbeya.
Amesema kilichoisibu Ihefu FC na kujikuta wanashindwa kufurukuta kwenye michezo kadhaa ya Ligi Kuu ni ukosefu wa muda mzuri wa kujiandaa na Ligi hiyo ambayo rasmi ilianza Septemba 06, huku akikosa muunganiko mzuri wa kikosi jambo ambalo lilimfanya ashindwe kupata matokeo chanya.
“Nilikua nimejipanga kufanya vizuri nikiwa na Ihefu FC, nakiri changamoto ya matokeo ilikua kubwa lakini niliamini ingemalizika kwa muda mfupi ujao na mambo yangenyooka. Kuondolewa kwangu hakumaanishi kama nina uwezo mdogo wa kufundisha.”
“Wote ni mashahidi kuwa sisi tulipanda kupitia michezo ya mtoani (Play-Off) na tulivyopanda tulijikuta tuna muda mchache sana wa kuandaa kikosi kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara ambayo nayo ilikuwa imechelewa kuanza kutokana na Janga la Virusi vya Corona ambalo lilikumba ulimwengu wote.” Amesema kocha Mwalwisi.
Mchezo wake wa kwanza alikubali kichapo cha mabao mawili kwa moja dhidi ya mabingwa watetezi Simba SC, Uwanja wa Sokoine, alishinda bao moja kwa sifuri dhidi ya Ruvu Shooting, kisha akapoteza dhidi ya Mtibwa Sugar kwa kufungwa mabao mawili kwa sifuri kabla ya kukutana na kichapo kama hicho dhidi ya Gwambina FC mwishoni mwa juma lililopita jijini Mwanza.
Kwa matokeo hayo Ihefu FC inashika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa kujikusanyia alama tatu.