Mwenyekiti wa klabu ya Young Africans Dkt. Mshindo Mbette Msolla amezungumzia mabadiliko katika benchi la ufundi la klabu hiyo, baada ya kuondolewa kwa kocha kutoka Serbia Zlatko Krmpotic.
Akizungumza na viongozi wa benchi la Ufundi la wachezaji katika kikao maalumu, Dkt. Msolla amesema mabadiliko ya makocha ni jambo la kawaida kwa timu inayohitaji mafanikio hivyo wachezaji na makocha wengine wasiingiwe na kihoro kwa jambo hilo.
“Kuondoka kwa kocha isiwe sababu ya kuwatia unyonge, muhimu ni kwamba mliopo tunaamini katika uwezo wenu hivyo muendeleze kazi nzuri wakati huu ambao anatafutwa kocha mkuu mwingine”.
“Kwa wachezaji hili lisiwatie wasiwasi mnafahamu kuwa timu inayohitaji mafanikio na inayojijenga kuna wakati inapitia katika hatua ngumu kama hizi , ” amesema .
Aidha Dkt . Msolla amewataka Wanachama , Wapenzi na Mashabiki wa Yanga , kuendelea kuwaunga mkono viongozi na kuisapoti timu yao kwa hali na mali katika kipindi hiki ambacho wanapambania kurejesha heshima Jangwani .