Wanasiasa wanaounga mkono demokrasia Hong Kong, wamejiuzulu kwa wingi baada ya wenzao wanne kufukuzwa katika Bunge la jimbo hilo, chini ya sheria ya China inayowakataza wanasiasa wanaounga mkono harakati za uhuru kushika wadhifa.
Taarifa iliyotolewa na mamlaka katika jimbo la Hong Kong imeeleza kuwa wabunge hao wanne Kwok Ka-ki, Alvin Yeung, Dennis Kwok na Kenneth Leung, wamefukuzwa bungeni kwa kuhatarisha usalama wa taifa.
Awali wanachama 19 wa upinzani walisema watajiuzulu kwa maandamano na walithibitisha kwamba watawasilisha barua za kujiuzulu Alhamisi.
Shirika la habari la China Xinhua limesema kupigwa marufuku kwa wanasiasa hao kumefuatia mikutano ya kamati ya kudumu ya Bunge ya watu wa China kupitisha azimio la kuwazuia wale wanaounga mkono uhuru wa Hong Kong au kukataa kukiri uhuru wa China juu ya mji huo.
Chini ya sheria hiyo mpya kuwauliza watu wa nje kuingilia masuala ya eneo hilo pia ni marufuku, kama ilivyo kitendo chochote kinachotishia usalama wa kitaifa.