Mabingwa wa soka nchini England Liverpool wameingia kwenye vita ya kumuwania beki wa kati kutoka nchini Ufaransa Dayotchanculle Oswald Upamecano.
Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp amemtaja beki huyo mwenye umri wa miaka 22, kama chaguo lake la kwanza baada ya kuumia kwa Joe Gomez aliyekuwa akiitumikia timu ya taifa ya England.
Kuumia kwa Gomez kuongeza matatizo katika safu ya ulinzi ya Liverpool, na kupelekea meneja Klopp kujipanga kuingia sokoni wakati wa dirisha dogo la usajili mapema mwakani.
Gazeti la Athletic liliripoti kuwa Upamecano anaongoza katika orodha ya Klopp, hasa baada ya kuumia kwa Gomez aliyeungana na Virgil Van Dijk katika benchi la wachezaji majeruhi.
Liverpool iliripotiwa kutaka kumsajili Upamecano msimu ujao, lakini sasa watahitaji kumsajili mapema kuziba pengo lililopo.
Hata hivyo Liverpool watapata upinzani katika harakati za usajili wa beki huyo wa klabu ya RB Leipzig ya Ujerumani, kufuatia benchi la ufundi la Manchester United kuonyesha dhamira ya kumuhamishia Old Trafford.
Manchester United wamejipanga kumsajili Upamecano, ikiwa ni sehemu ya kutaka kuboresha kikosi chao, ili kurejesha heshima kama ilivyokua zamani.