Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi leo Desemba 8 atamuapisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.
Hafla ya kumuapisha Maalim Seif itafanyika Ikulu Zanzibar.
Desemba 6, mwaka huu Rais Mwinyi alimteua Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Hata hivyo wadhifa huo si mpya kwa mkongwe huyo wa siasa za Tanzania.
Kabla ya mtafaruku wa kisiasa baada ya kufutwa matokeo ya uchaguzi wa 2015, Maalim Seif akiwa Chama cha Wananchi (CUF) alihudumu katika nafasi hiyo kutoka mwaka 2010 hadi 2015. Wakati huo Dkt. Ali Mohammed Shein wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwa Rais.
Uteuzi huo umezingatia matakwa ya kifungu cha 9(3) cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.