Aliyekua kocha mkuu wa Namungio FC Hitimana Thiery amekamilisha dili la kujiunga na Mtibwa Sugar, ikiwa ni majuma kadhaa baada ya kusitishiwa mkataba wake na waajiri wake wa zamani.
Taarifa kutoka Manungu, Tuariani mkoani Morogoro zinaeleza kuwa, kocha huyo kutoka nchini Rwanda, amekamilisha mpango huo baada ya kumaliza mazungumzo na viongozi wa Mtibwa Sugar, ambao walionesha nia ya kufanya naye kazi tangu alipotangazwa kuondoka Namungo FC.
Kocha huyo ambaye ana uzoefu na Ligi Kuu Bara anarithi mikoaba ya Zuber Katwila ambaye alitimkia Ihefu FC ya mkoani Mbeya.
Kabla ya dili hilo kukamilika, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru alithibitisha mchakato wa kutangazwa kwa kocha mpya ulikua njiani, na viongozi wake walikua wanawajadili baadhi ya makocha ambao walionekana wanafaa kukinoa kikosi cha klabu hiyo kongwe kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Hapa Mtibwa Sugar ni chuo na wengi wanapenda kuja kufundisha ndani ya timu hii hivyo mambo yakiwa sawa tutamtangaza yule ambaye atakuja kuwa kocha mkuu ndani ya kikosi chetu.”
“Kuhusu Hitimana,(Thiery) kwa sasa sijajua kama ni miongoni mwa wale ambao wameomba kazi ndani ya Mtibwa Sugar, tunaamini tutaweka wazi mambo haya bila tatizo,” Alisema Kifaru
Hitimana anaendelea kuwa sehemu ya makocha wa soka la Bongo, akifanya kazi kwa zaidi ya miaka mitatu, alipowasili nchini alianza kuwa na kikosi cha Biashara United Mara, kisha aliajiriwa Namungo FC na sasa yupo Mtibwa Sugar.
Mtibwa Sugar ipo nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikifikisha alama 19, baada ya kushuka dimbani mara 15, huku ikifunga mabao 7 na kufungwa 9.