Jumla ya wanafunzi 759,706, sawa na asilimia 91.1 ya wanafunzi waliofaulu wakiwemo wavulana 368,174 na wasichana 391,532 wamechaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2021.
Hilo limebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo wakati akitoa taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2021 leo jijini Dodoma.
Jafo amesema kuwa kati ya hao wanafunzi, 4,169 wamechaguliwa kujiunga na shule za bweni ambapo wanafunzi 970 watajiunga na shule za wanafunzi wenye ufaulu mzuri zaidi.
Aidha, Jafo amesema kuwa wanafunzi 1,238 watajiunga na shule za ufundi, wanafunzi 1,961 watajiunga na shule za bweni za kawaida.
Wanafunzi 755,537 wakiwemo wavulana 362,247 na wasichana 385,665 wamechaguliwa kujiunga na shule za Sekondari za kutwa katika maeneo mbali mbali nchini.
“Miongoni mwa waliochaguliwa, wanafunzi wenye mahitaji maalum ni 2,491 wakiwemo wavulana 1,312 na wasichana 1,179 sawa na asilimia 75.0 ya wanafunzi wenye ulemavu waliofanya mtihani huo,” amesema Jafo.
Jafo ameeleza kuwa jumla ya mikoa tisa ya Kagera, Katavi, Lindi, Mtwara, Mwanza, Njombe, Ruvuma, Songwe na Tabora imeweza kupangia shule wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.
Hata hivyo jumla ya wanafunzi 74,166 sawa na asilimia 8.9 wakiwemo wavulana 34,861 na wasichana 39,305 hawakupangiwa shule katika awamu ya kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
“Hivyo wanafunzi wenye sifa ambao hawakupangiwa shule katika awamu hii ya kwanza watapangiwa shule katika awamu ya pili kabla ya tarehe 28 Februari, 2021”, ameeleza Waziri Jafo.