Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amebainika kuwa na virusi vya corona (covid-19) baada ya majibu ya vipimo kuwekwa hadharani leo, Desemba 17, 2020.
Ikulu ya nchi hiyo imeeleza kuwa Rais Macron alionesha dalili za awali za maambukizi, hivyo timu ya madaktari ikalazimika kumfanyia vipimo vya PCR.
Msemaji wa Ikulu, Sibeth Ndiaye amesema kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa Rais huyo atawekwa katika eneo maalum la kujitenga (karantini) kwa kipindi cha siku saba lakini ataendelea kuiongoza nchi akiwa huko.
Ameeleza kuwa safari zote za hivi karibuni za Rais Macron zimeahirishwa ikiwa ni pamoja na ziara yake nchini Lebanon iliyopangwa kufanyika Desemba 22.
Aidha, Waziri Mkuu Jean Castex na Spika wa Bunge, Richard Ferrand pia watalazimika kuwekwa karantini kwakuwa walikutana na Rais Macron katika siku za hivi karibuni, kwa mujibu wa mkuu wa Baraza la Seneti, Gerard Larcher.
Bado haijafahamika Rais Macron alipataje virusi hivyo, lakini ofisi yake imesema inaendelea kufanya utafiti kupitia watu aliokutana nao hivi karibuni.
Ufaransa ni moja kati ya nchi zilizoathirika zaidi na covid-19, ambapo wiki hii iliweka sheria ya kutotembea usiku ili kupambana na kasi ya kusambaa kwa maambukizi.
Hadi sasa zaidi ya watu milioni mbili wamethibitika kupata maambukizi ya covid-19 na vifo zaidi ya 59,400, kwa mujibu wa takwimu za Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.