Shirika la Water Mission Tanzania kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) limezindua mradi wa maji kwa Wakazi wa Kata ya Msamalo,Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma amabpo wakazi zaidi ya 4000 watanufaika na mradi huo pamoja na taasisi za kijamii kwenye eneo hilo.
Akizindua mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandishi Antony Sanga amesema kukamilika kwa mradi huo ni utekelezaji wa ahadi za Serikali katika kupunguza kero ya maji kwa wananchi na kwamba utasaidia kuboresha maisha ya wakazi wa eneo hilo.
“Tunamshukuru sana Rais wetu, wakati wa kampeni aliahidi kwamba tutawapelekea wananchi wetu huduma ya maji hivyo huu ni upendo wake kwenu wana Msamalo,” amesema Mhandishi Sanga.
Aidha amewataka wakazi wa Msamalo kushirikiana ili kuendeleza mradi huo ili uwe endelevu kwa manufaa kwa vizazi vijavyo.
Naye Mkurugenzi wa Water Mission Tanzania, Benjamin Filskov alisema utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa shirika hilo katika kuunga mkono jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata maji safi na salama karibu na makazi yao.
“Tunatambua uwepo wa mahitaji makubwa ya maji kwenye eneo hili na leo hii tunayo furaha kuzindua mradi huu ambao utasaidia kupunguza adha ya maji kwa wakazi wa eneo hili, mafanikio haya ni ishara ya ushirikiano wet una Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) na Wizara ya Maji katika kusaidia jitihada za Serikali kufikisha huduma za maji kwa watu wote,” amesema Filskov
Mradi huo unaotumia nishati ya jua ‘Solar’ ambapo maji yanavutwa kutoka kwenye kisima na kwenda kwenye kituo cha kusafisha na kutibu maji na baadaye yanapelekwa kwenye vituo 18 vilivyopo karibu na makazi ya watu.