Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC wameondoka nchini leo Ijumaa kuelekea Zimbabwe, kwa ajili ya kuwavaa FC Platinum kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaopigwa Jumatano Desemba 23.
Simba itacheza na timu hiyo ya Zimbabwe, baada ya kupenya hatua ya awali kwa kuitoa Plateau United ya Nigeria kwa ushindi wa bao 1-0 walilolipata kwenye mchezo wa ugenini, kabla ya kulazimishwa suluhu kwenye mchezo wa pili uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Akizungumza kabla wa kuondoka Dar es salaam, kocha mkuu wa Simba SC Sven Vandenbroeck alisema wanakwenda Zimbabwe kupambana ili kupata matokeo yatayowaweka kwenye mazingira mazuri ya kutinga kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo kocha Sven alisema anaamini mchezo dhidi ya FC Platnum hautokua rahisi , lakini atawahimiza wachezaji wake kupambana kama ilivyokua kwenye mchezo dhidi ya Plateau United ya Nigeria.
“Hautakuwa mchezo mwepesi, tunakwenda kupambana ili kufanya vizuri, hii ni Ligi ya Mabingwa Afrika huku kuna ushindani mkubwa tofauti na ligi,” alisema Sven.
Naye beki wa Simba, Shomari Kapombe alisema wamekwenda Zimbabwe kupambana na kutafuta matokeo mazuri katika mchezo wao dhidi ya FC Platinum, ana amini kwamba utakuwa mchezo wa ushindani kwa sababu kuna baadhi ya nyota waliwahi kucheza soka Tanzania.
“Utakuwa mchezo mgumu kwa sababu kuna baadhi ya wachezaji ambao wamewahi kupita na kucheza soka hapa nchini akiwamo Thaban Kamusoko na Elius Maguli ambaye naye aliwahi kucheza Simba,” alisema Kapombe.
Simba watacheza mchezo wa kwanza ugenini Desemba 23 na ule wa marudio unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa Januari 06.