Vikosi vya usalama vimewaokoa wanafunzi 344 wa kiume waliotekwa nyara na wanamgambo wa itikadi kali Kaskazini mwa Nigeria katika msitu wa Rugu, jirani na jimbo la Zamfara.
Katika operesheni hiyo ya uokozi, vikosi vya usalama vililizingira eneo ambalo vijana hao walikuwa wanashikiliwa na watekwaji na hatimaye kuwaokoa vijana hao.
Gavana wa jimbo la Katsina Aminu Bello Masari amesema wavulana hao wamepelekwa katika jimbo la Katsina na kukabidhiwa kwa familia zao baada ya kufanyiwa uchunguzi wa matibabu.
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amepongeza kuachiwa kwao, akisema ni ahueni kubwa kwa familia zao, nchi nzima na kwa jamii ya kimataifa.
Kundi la Boko Haram chini ya kiongozi wake Abubakar Shekau lilidai kuhusika na utekaji nyara huo wa Ijumaa wiki iliyopita katika shule moja ya sekondari ya serikali, katika mji wa Kankara jimboni Katsina.